Jumatano , 26th Mar , 2014

Shirikikisho la wachimbaji na watafutaji madini na nishati nchini Tanzania TCME, limelaani vikali maandamano ya wachimbaji waliokuwa wakichimba dhahabu katika eneo la Mwashina, wilayani Nzega mkoani Tabora yaliyofanyika siku chache zilizopita.

Mbunge wa Nzega Dkt Khamis Kigwangala akiwa amekamatwa na polisi wakati wa vurugu za wachimbaji wadogo wadogo zilizotokea jimboni mwake hivi karibuni.

Katika taarifa yao leo kwa vyombo vya habari, TCME limesema si vyema wananchi wakajenga chuki dhidi ya wawekezaji kama walivyofanya wachimbaji hao wadogo, na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaweza kuchochea machafuko na pia kudhoofisha juhudi za dhati za Serikali za kukuza uchumi kwa kuvutia wawekezaji.

Mjumbe wa TCME Bw. Rodgers Senziga amesema shirikisho hilo linatoa rai kwa serikali kusimamia sheria na kuendelea kutenga maeneo halali kwa ajili ya wachimbaji wadogo pamoja na kuratibu shughuli za wachimbaji wadogo ili ziwe endelevu na kuchangia vema katika uchumi wa taifa na kuepusha migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.