Ijumaa , 23rd Mei , 2014

Kambi rasmi ya upinzani bungeni nchini Tanzania imeitaka serikali iwawezeshe wabunge wanaoiwakilisha Tanzania katika bunge la Afrika Mashariki kwa kuwapa ofisi pamoja na kuwapatia vitendea kazi vitakavyowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Freeman Mbowe.

Wito huo umetolewa bungeni mjini Dodoma na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani na mbunge wa jimbo la Hai Mh. Freeman Mbowe wakati alipokuwa akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti kwa wizara ya ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mh. Mbowe amesema inashangaza kuona kwamba serikali ya Tanzania inashindwa kuona fursa zilizopo katika nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki na kupelekea baadhi ya nchi hizo kuishangaa Tanzania kwa kushindwa kutumia fursa hizo.