Jumanne , 27th Oct , 2015

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesema kuwa zoezi la kupiga kura liliendeshwa vizuri na kwa uwazi japo kulikuwa na mapungufu kidogo kwenye baadhi ya maeneo.

Mh. Moody Awori Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kiongozi wa ujumbe huo Mh. Moody Awori amesema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa kipekee kwani ulikuwa na ushindani mkubwa toka wakati wa kampeni na watu wengi wamejitokeza kupiga kura katika hali ya amani na utulivu japo kuna vituo vichache vilivyorudia uchaguzi Oktoba 26.

Awori ameongeza kuwa hii ni ripoti ya awali na ripoti kamili ya uchaguzi wote wataitoa baada ya wiki mbili mpaka tatu baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya urais.

Aidha Awori amesema kuwa demokrasia imekuwa sana nchini Tanzania na kushauri kuwa mchakato wa katiba mpya uanze upya mara moja baada ya kuisha uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa michakato ya uchaguzi pamoja na kuwa na tume huru.