Ijumaa , 13th Feb , 2015

Vurugu zimetokea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe baada ya hoja ya madiwani katika halmashauri hiyo kumkataa mwenyekiti wao mh. Abel Mlala kupingwa.

Vurugu zimetokea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe na kulazimu jeshi la polisi kuingilia kati baada ya hoja ya madiwani katika halmashauri hiyo kumkataa mwenyekiti wao mh. Abel Mlala kupingwa hali iliyosabisha mvutano na kuvunjika kwa kikao.

Vurugu hizo zilianza mara baada ya mwenyekiti kufungua kikao ambapo madiwani walishinikiza kujadiliwa kwa hoja ya kumkataa na ndipo yalipozuka malumbano ya hoja kati ya madiwani na mwanasheria wa halmashauri hiyo Barichako Nzaniye, hali iliyosababisha kuahirishwa kwa kikao hicho na polisi kuamuru watu wote kutawanyika kutokana na kuwepo kwa viashiria vya kuvunjika kwa amani.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Abel Mlala na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Buhigwe Simon Mumbee walieleza kuwa madiwani hao hawajafuata utaratibu katika kuwasilisha hoja yao hivyo hakuna sababu ya kuendelea na kikao huku kukiwa hakuna utulivu na kuna dalili za kuvunjika kwa amani.

Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe imekuwa na mgogoro kwa karibu miezi sita sasa ambapo madiwani wa halmashauri hiyo wamekuwa wakidai kutokuwa na imani na mwenyekiti wao kwa madai ya kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo, madai ambayo yamekuwa yakipingwa na mwenyekiti .