
Ahadi ya visiwa hivyo kupelekewa umeme imetolewa na waziri wa nishati Januari Makamba kufuatia ziara ya siku tatu aliyoifanya mkoani Kagera kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili wananchi kutokana na kukosa nishati hiyo, wakiwamo wanaoishi na kufanya biashara visiwani.
"Mimi nataka niwaahidi wajomba zangu wawili hapa, basi kama ni hivyo Muleba Kusini nitakuwekea umeme katika visiwa vinne na Muleba Kaskazini Visiwa vinne kwa kuanzia kwa sababu hii programu ni endelevu, kwa hiyo inabidi mkae na REA mchague pa kuanzia ni wapi" amesema.
Naye mkuu wa wilaya ya Muleba, Toba Nguvila amesema kuwa hitaji la umeme kwa wananchi wanaoishi visiwani ni kubwa, na kumuoma waziri Makamba kusaidia kuwaondolea kero hiyo ambayo inakwamisha maendeleo ya wananchi.
"Tunahitaji umeme kwenye vitongoji na vijiji vyake 26 ambavyo wanaishi watu takriban 100,000, Pangani ni Wilaya ina watu 63,000 lakini hapa visiwa tu peke yake vina watu 100,000, hata mimi DC kufanya ziara visiwani lazima nijipange" amesema Nguvila.