Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, DCP Ahmed Msangi wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake na kuwataja watu hao kuwa ni Deus Lucas diwani wa kata ya Mabatini chadema, Daniel Mongo Mwenyekiti chadema tawi la Kiloleli B', Laurence Chilo, Lameck Kaunda.
Wengine ni Jackson Madebe, Bi Secilia Butuko, Mwita Sagali na Selemani Gabriel ambapo wote hao walikamatwa Machi 13, 2018 majira ya saa 10:30 jioni ndani ya nyumba ya Laurence Chilo wakiwa wamefunga bendera za chama chao na kuweka spika za matangazo huku wanachama hao wakidai walikwenda kuhani msiba wa mwanachama mwenzao aliyefiwa na mama yake mzazi miezi sita iliyopita.
Aidha, Kamanda Msangi amesema katika tukio hilo wameweza kupata bendera ya Chadema, kadi za chama hicho zilizoandikwa majina nusu na nyingine hazijaandikwa majina, mihuli miwili, karatasi tatu zenye majina ya mahudhurio na T-shirt zenye nembo ya Chadema.
Kwa upande mwingine, DCP Msangi amesema Jeshi la Polisi lipo katika upelelezi na mahojiano dhidi ya watuhumiwa hao na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.