Jumamosi , 28th Jul , 2018

Vijana wengi wanadhaniwa kuja kupoteza ajira kutokana na agizo la Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim  la kuwataka madereva wanaoendesha vyombo vya moto kuwa na leseni pamoja vyeti vya udereva vilivyotolewa na vyuo vinavyojulikana na serikali.

Picha hii haina mahusiano ya moja kwa moja na habari.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bodaboda Taifa, Bw. Rashid Omar Faru, wakati akifanya mazungumzo na www.eatv.tv ambapo amesema kwa uelewa wake wa kufanya kazi na serikali anafahamu vijana wengi wanaoendesha bodaboda hawana vyeti vinavyohitajika na serikali.

Bw. Faru ameongeza, kitendo cha Kamanda Muslimu kufanya ukaguzi huo ambao yeye anauunga mkono, kitasababisha vijana wengi kurudi mitaani na kushindwa kutekeleza agizo la hapa kazi tu la Rais Magufuli ambaye anataka vijana wasibweteke.

"Serikali ya Rais Magufuli inataka vijana wajitume, wafanye kazi wasikae mitaani. Bodaboda na bajaji imekuwa ajira kubwa kwa vijana. Nina wasiwasi kwamba wengi watakosa ajira kwa hili litakalokwenda kufanyika, lakini ni lazima wafuate sheria ambayo serikali wameiweka, ila inabidi pia serikali watusikilize na sisi madereva wakae mezani na sisi tueleweshane" amesema Faru.

Pamoja na hayo Bw. Faru amewataka vijana kutoishi kwa mazoea bali wanapaswa kuchangamkia fursa zilizopo na kuwakumbusha kwamba zama zimebadilika.

Hivi karibuni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Muslim alitangaza kufanya operesheni kwa madereva wasiokuwa na vyeti pamoja na leseni na kwamba hatakubali madereva wenye vyeti visivyokidhi vigezo kuingia barabarani.