Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Davis Mwamunyange
Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Davis Mwamunyange amewataka vijana wanaomaliza mafunzo ya jeshi na kukosa nafasi za ajira kutumia mafunzo mbalimbali wanayoyapata JKT hasa ya stadi za kazi kuelimisha wengine ikiwa ni pamoja na kudumisha amani katika maeneo wanayoishi.
Jenerali Mwamunyange ametoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa gwaride maalum la kuwaaga majenerali wastaafu zoezi lililofanyika viwanja vya kambi ya Twalipo Mgulani ambapo amesema vijana wanapoingia jeshini mbali na kupewa mafunzo ya kijeshi lakini pia wanapata mafunzo mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo, ufundi wa aina mbalimbali ili wanapohitimu waweze kujitegemea huku wakiwataka maofisa wengine kufuata nyayo za waliostaafu.
Kwa upande wao baadhi ya majenerali waliostaafu wamesema kwa sasa jeshi limepiga hatua kiteknolojia tofauti na wao walivyojiunga na jeshi na kuongeza kuwa ni bora kuwa na jeshi dogo lakini la kitaalam huku wakiwataka wanaoandikisha vijana kuingia jeshini kuhakikisha wanakuwa waadilifu wakati wa kuchuja ili kupata vijana wenye vigezo.
Sherehe hizo zimepambwa na mazoezi mbalimbali likiwemo gwaride maalum la kuwaaga wastaafu hao pamoja na zoezi la wao kukabidhi vitambulisho vyao vya kazi kwa mkuu wa majeshi na yeye kuwakabidhi vitambulisho vya kwenda uraiani pamoja na funguo za gari ambayo yametolewa na jeshi baada ya kulitumikia kwa kwa uadilifu muda wote huo.