Wito huo umetolewa na Mkuu wa mafunzo ya kujenga uwezo kutoka Asasi ya Tanzania Youth Vision Association Bi. Dianarose Leonce, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Supermix kinachorushwa na East Africa Radio.
Bi. Leonce amesema vijana wengi wameonyesha kuwa na mwamko wa kufuatilia masuala ya kisiasa yanayoendelea kwa sasa hapa nchini, lakini wengi wao wanafuatilia wakiwa na ushabiki pasipo kufuatilia hoja za viongozi hao, huku kundi kubwa la vijana hao wakiwa bado hawajastaarabika hususan katika matumizi ya mitandao ya kijamii juu ya masuala ya kisiasa.
Pia Bi. Leonce amewataka vijana kujiunga na asasi mbali mbali za kiraia zinazotoa elimu mbali mbali kwa vija, kwani kwa kufanya hivyo watapata fursa ya kujifunza na kupata elimu kubwa juu ya masuala mbali mbali.
Nae kijana Abdul Lukanza ambae ni Afisa Ushiriki Vijana kutoka Asasi ya Restless Development, ametaka vijana washirikishwe kwenye utungaji wa sera zao, kwani kwa kushiriki kwao kutasaidia kutambua ni vitu gani wanataka toka kwa viongozi wao.
Pia Bwn. Lukanza amesema kuna uhitaji wa kuweka nguvu zaidi ili vijana wawe na uelewa zaidi na si ushabiki, pamoja na kuwa wawajibikaji katika masuala mbali mbali na kuacha kulaumu watu au mfumo fulani.



