Alhamisi , 8th Oct , 2015

Serikali imetakiwa kuandaa mazingira rafiki ya kuweza kuandaa vijana kushiriki katika masuala ya kisiasa, kwa sababu ndio mazingira pekee yanayoandaa viongozi wa baade.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa Fahimi Mastawili, alipokuwa akiongea kwa njia ya simu kwenye kipindi cha Super mix, kinachorushwa na East Africa radio, na kueleza kwamba kama vijana hawawekewi mazingira maalum ya kuweza kuwa viongozi baade, tutakuwa tunajidanganya.

"Serikali ijayo itengeneze mazingira rafiki ya kuweza kuwaandaa vijana kuweza kushiriki katika masuala ya kisiasa, kwa sababu ndio mazingira pekee yanayowaandaa viongozi wa baadae, sasa kama unasema vijana ndio Taifa la leo, mara la kesho, alafu hakuna mazingira maalum ya kuwaandaa vijana kuwa viongozi tutakuwa tunawadanganya", alisema Mastawili.

Mastawili amesema kwa sasa vijana wanayumba kwa sababu hawajatengenezewa mazingira ya kuwa viongozi, ingawa wamekuwa kwenye mchakato wa kuweza kuwawezesha vijana kuwa viongozi, lakini mpaka sasa hakuna mafanikio.

" Tumekuwa kwenye harakati kwa muda mrefu, na mimi pia kama mdau nimechangia kama 60% ya mchakato ambao leo tumepata sheria ya vijana wa vijana, vile ni vyombo maalum vya kuandaa vijana kuzungumza matatizo yao, kukaa na kujadiiana kuweza kuandaa vijana na kuwa viongozi wa baadae, lakini tunayumba kwa sababu hatujatengenezewa mazingira mazuri ya kuwa viongozi", alisema Mastawili.

Pia Fahimi Mastawili amesema vijana wanapoandaliwa kuwa viongozi si lazima kuwa viongozi wa kisiasa, bali wananweza wakawa viongozi kwenye Taasisi za umma, na kusaidia kuongoza jamii kwenye Taasisi hizo.