Jumanne , 15th Mar , 2016

Zaidi ya asilimia 21 ya kina Mama na watoto wamekuwa wakipoteza maisha kila mwaka wilayani Bahi Mkoani Dodoma kutokana na ukosefu wa huduma ya dharura ya upasuaji kwa kina mama wajawazito.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu

Mganga Mkuu wa Halmshauri ya Bahi, Dkt. Reina Kapinga amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo wameamua kuchukua hatua za awali za kuanzisha ujenzi wa chumba cha upasuaji ili kutatua changamoto hiyo.

Dkt. Reina amesema ingawa idadi ya vifo vya kina mama inaonyesha kupungua toka 290 kwa miaka 10 iliyopita hadi kufikia 272 kwa vizazi hai laki moja mpaka kufikia mwaka jana lakini bado hawajafikia malengo ya Milenia ya kupunguza vifo hivyo.

Katika kuunga mkono jitihada za serikali katika uboreshaji wa huduma za Afya wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia chumba cha upasuaji katika Halmshauri hiyo ili kupunguza na hatimae kutokomeza kabisa tatizo hilo.

Wilaya hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2007 mpaka hivi sasa haina Hospitali ya wilaya hali ambayo imefanya wananchi wa wilaya hiyo kufuata huduma za afya katika vituo vya afya ambavyo hata hivyo havitoshelezi mahitaji.