Ijumaa , 1st Jul , 2016

Zaidi ya vibanda mia tano (500) vidogovidogo vinavyotumiwa kama makazi ya biashara na` wafanyabiashara wadogowadogo wa maeneo ya kisiwa kidogo cha Kabiga na migongo vimeteketea kwa moto katika matukio mawili tofauti wilayani Sengerema.

Taarifa ya jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza imeeleza kwamba tarehe 30.06.2016 majira ya saa 8:00 mchana katika kisiwa cha kabiga kata ya Maisome tarafa ya Kahunda wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza, vibanda zaidi ya mia tatu [300], vimeteketea kwa moto, na kusababisha hasara ya mali na vitu ambavyo haijafahamika thamani yake mpaka sasa.

Vibanda hivyo vidogovidogo vilivyoshikana vilivyojengwa kwa mabanzi ya miti na kuezekwa kwa karatasi za nailoni vinatumiwa kama makazi ya biashara na wakazi wa maeneo hao.

Inadaiwa kuwa moto huo uliwashwa na watu wasiofahamika wakati wakigawana mafuta aina ya petrol karibu na kibanda kilichopo maeneo hayo, ambapo inasemekana walikua wameyaiba sehemu nyingine.

Imedaiwa wakati wa tukio hilo mmoja kati yao alikuwa akivuta sigara hali iliyopelekea mafuta hayo ya petrol kulipuka na kuteketeza vibanda vyote katika eneo hilo na watu hao kutoroka kusikojulikana .

Aidha katika tukio lingine la ajali ya moto la tarehe tajwa hapo juu majira ya saa 04:00 usiku katika kisiwa cha Migongo kata ya Maisome wilayani Sengerema, zaidi ya vibanda mia mbili [200] ambavyo navyo pia vilikuwa vimejengwa kwa mabanzi ya miti na kuezekwa kwa karatasi za nailoni vinavyotumiwa kama makazi ya biashara na wakazi wa maeneo tajwa hapo juu navyo viliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mali na vitu kwa wafanya biashara wa sehemu hiyo.

inasemekana kuwa moto huo ulianzia kwenye kibanda cha mfanyabiashara mmoja aliyejulikana kwa jina moja la dotto aliyewasha mshumaa ndani ya kibanda chake na kwenda kwenye matembezi yake ya kawaida, ndipo mshumaa ulipolipuka na kuunguza kibanda chake chote kisha moto huo kusambaa katika vibanda vingine.

Aidha hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha au kujeruhiwa katika ajali zote mbili, jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi pamoja na msako wa kuwasaka wahusika wanaodaiwa kuwa ndiyo chanzo cha ajali hizo za moto, mpaka sasa thamani ya vitu na mali zilizoteketea kwa ajali hizo za moto bado hazijafahamika.

Kamanda wa Polisi Mkao wa Mwanza Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo akiwataka kuwa makini na kuacha kuishi kimazoea, lakini pia kuacha kuwa na mazoea na watu ambao wanatabia za uhalifu ambao wanasababisha hasara kubwa kwa wananchi wengine.