Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya chakula na lishe Tanzania TFNC Dkt. Abbas Kimboka amesema ili kuondokana na tatizo hilo ni vyema jamii ikajenga tabia ya kuwawezesha kinamama wajawazito kupata lishe bora nyakati za ujauzito na kipindi cha kunyoshe sambamba na kuwapunguzia kazi ngumu.
Dkt. Kimboka amesema, madhara ya utapiamlo hubainika pale mtoto anapokuwa na uzito mdogo na udumavu tofauti na umri wake lakini pia madhara hayo huambatana na magonjwa na kupungukiwa damu kwa watoto hali ambayo isipodhibitiwa chini ya miaka 2 huleta madhara makubwa baadaye.
Afisa lishe wa watoto wachanga na wadogo kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania TNFC Bi Neema Joshua amesema magonjwa mengi ya figo, magonjwa ya moyo na kisukari yanayowakabili watu wengi ukubwani chanzo chake ni lishe duni nyakati za utoto.
“Watu hawana lishe bora tangu utotoni wamekuwa wakubwa maisha yamebadilika lakini bado mwili umedumaa tangu awali, wataalam wanahusisha magonjwa ya figo, kisukari na moyo huchangiwa na utapiamlo utotoni” amesema
Kundi pekee ambalo litaisaidia taifa kuondokana na madhara ya utapiamlo na kufikiwa kwa maendeleo endelevu ni pale tu akinamama wajawazito na wanaonyonyesha watakapopewa lishe bora na kupunguziwa kazi ngumu nyakati za malezi ya watoto ili taifa liondokane na asilimia 34 ya watoto wenye utapia mlo.
Mikoa ya Geita, Njombe, Iringa na Kagera ikitajwa kuwa ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini lakini imetajwa kuwa na kiwango kikubwa cha utapiamlo kutokana na jamii kushindwa kuwekeza kwenye lishe na afya ya watoto licha ya kuwepo chakula.




