Halmashauri ya wilaya ya Mufindi inayopambana kupandisha kiwango cha elimu katika shule zake za msingi inakabiliwa na changamoto mbalimbali kufikia malengo hayo ikiwa ni pamoja na imani za ushirikina na mwamko mdogo wa wazazi katika masuala ya elimu.
Baadhi ya walimu kutoka katika shule za msingi zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani iliyofanyika Oktoba mwaka jana wamesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatishia watoto wao kwa kuwaagiza kutojaza majibu ya kweli kwenye mitihani yao, kwa maelezo kuwa wakifanya vizuri na kufaulu mitihani hiyo watarogwa.
Afisa Elimu wa halmashauri ya Mufindi, amesema wilaya hiyo yenye jumla ya shule za msingi 177 imekuwa ikishikilia nafasi ya pili katika kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba kimkoa na kupandisha wastani wa ufaulu kutoka asilimia 38.9 mwaka 2012 hadi asilimia 68.2 mwaka 2014.
Katika kikao hicho cha tathimini ya elimu wilayani Mufindi, mwenyekiti wa halmashauri hiyo Peter Tweve amekabidhi zawadi ya pikipiki kwa shule ya msingi holo kwa kufanya vizuri katika matokeo hayo ya mitihani ya mwaka jana kama motisha.
Shule hiyo imekuwa na rekodi ya kufaulisha wanafunzi wake kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kipindi cha miaka sita mfululizo.