Ijumaa , 28th Oct , 2016

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya amewataka wajumbe wa Kamati ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kuweka mikakati imara ya kupambana na wahalifu wa biashara hiyo nchini.

Wajumbe wa kamati ya kupambana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu nchini.

 

Akizungumza kabla ya kufungua mkutano wa wajumbe hao wenye lengo la kujadili na kutengeneza mkakati wa kukabiliana na biashara hiyo, Balozi Simba alisema biashara hiyo imekuwa ikiongezeka duniani na wahalifu wakipata faida ya mabilioni ya fedha kutokana na wahanga, wengi wao wakiwa ni watoto, ambao huporwa utu na uhuru wao.

“Inawezekana wengi wetu hatujakutana na aina hii ya uhalifu, lakini unatokea kila siku duniani kote, na nchi yetu ni mojawapo kati ya nchi zinazoathirika na tatizo la biashara hii haramu,” alisema Balozi Simba na kufafanua;

“Tanzania ni chanzo, njia ya kupitia na pia hupokea wahanga wa biashara hii haramu. Wahanga hawa husafirishwa kutoka maeneo ya vijijini kwenda mijini hapa nchini, wengine husafirishwa kwenda Ulaya, Marekani, Asia na nchi za Kiarabu kama vile Oman na Dubai.”

Alisema watu hao hudanganywa kwa ahadi za kupata ajira nzuri au nafasi za elimu, lakini mwisho wake huishia kunyonywa, kuwa watumwa wa ndani na kufanyishwa kazi kwa nguvu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, Vincent Magere, alisema kikao hicho kinawahusisha Wajumbe wa Kamati na Sekretarieti kutoka Bara na Visiwani ambapo wanakutana kwa mujibu wa sheria ambapo wanapaswa kukutana mara tatu au nne kwa mwaka.