Jumatano , 9th Dec , 2015

Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za afya na elimu kwa haraka.

Akizungumza mara baada ya kushiriki kufanya usafi katika kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania bara kama alivyoagiza Rais wa Tanzania, Mhe. Suluhu amesema wananchi wajenge tabia ya kufanya usafi kwa hiari ili kuondokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Aidha, Makamu wa Rais amewapongeza waliojitokeza katika zoezi hilo na kuwataka wananchi waendelee na zoezi hilo sio mpaka siku ya Uhuru tu ili kuwasaidia wananchi kuondokana na ujinga pamoja na maradhi yanayowakabili pamoja na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa aliyefanya usafi katika soko la Kariakoo amewataka viongozi wa soko la Kariakoo wafike ofisini kwake Jumatatu ijayo ili wamueleze wana mikakati gani ya kuboresha utoaji huduma kwenye soko hilo.