Jumapili , 29th Mei , 2016

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Serikali kutimiza ahadi yake ya kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini kama ilivyo Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ili kusimamia utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa vijijini.

Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo jana , Msemaji katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Hamidu Bobali, alisema mradi wa kuvipatia maji vijijini 10 kwa kila wilaya ulitumia fedha nyingi lakini hayakupatikana.

Alisema visima vingi vilichimbwa wakati maeneo husika hayajafanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa baadhi ya watendaji wa halmashauri waliiba fedha za mradi huo wakidai wamejenga visima vya maji huku akisisitiza kwamba visima vingine vilijengwa na taasisi za kidini au za kijamii.

Kwa upande wake Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeitaka Serikali imetaka Serikali ifanye marekebisho kwenye sheria ya fedha ya mwaka 2016 kwa kuweka tozo ya Sh100 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli na kuelekeza fedha hizo kwenye Mfuko wa Taifa wa Maji.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Christine Ishengoma alisema fedha zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zimekuwa hazitolewi kwa wakati, hivyo kukwamisha utekelezaji wa miradi iliyopangwa.