Jumapili , 22nd Nov , 2015

Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu wa ngozi wamezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinakomesha mara moja, ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye albinism sambamba na kutoa huduma za kliniki

na matibabu kwa watu wenye albinism na ambao wameathirika na mionzi mikali ya jua.

Mkurugenzi wa Shirika linalotetea haki za watu wenye albinism nchini Tanzania la Under The Same Sun, Bi. Vicky Ntetema, amesema hayo leo wakati akitoa maazimio ya washiriki wa mkutano huo.

Ntetema amesema mojawapo ya maazimio ni pamoja na kuundwa kwa mtandao wa watu wenye albinism barani Afrika, mtandao ujulikanao kama Pan African Albinism Network utakaowasaidia kupata huduma na elimu ya kutosha kuhusiana na jinsi ya kujilinda na madhara yatokanayo na jua na kuendelea na shughuli zao za kawaida kama binadamu wengine.

Ameongeza kuwa moja na mafunzo waliyopata ni pamoja na ni jinsi ya kuzuia kupata saratani ya ngozi na huduma za klinik za uoni hafifu wenye lengo la kusaidia wanafunzi na watu wengine kufanya kazi kwa ufasaha.

Waliokuwepo katika mkutano huo ni pamoja na wataalamu wa afya na wanasaikolojia ambao walitoa mafunzo jinsi ya kuwahudumia walemavu wa ngozi na kuweka mkakati wa kuwa mabalozi katika nchi zao katika kutetea haki za watu wenye Albinism.