Jumamosi , 16th Mei , 2015

Serikali imesema kuwa uchaguzi mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania uko palepale na utafanyika wiki ya mwisho wa mwezi wa kumi ambapo dafatri la kudumu la mpiga kura litakua limekamilika.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda akijibu maswali mbalimbali Bungeni.

Akizungumza leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotelewa katika mjadala wa kujadili bajeti ya ofisi ya waziri mkuu, waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda amesema kuchelewa kutolewa kwa fedha za uandikishaji kwa Tume ya Uchaguzi hakukua na nia ya kusogeza uchaguzi mbele.

Aidha waziri mkuu amesema kuwa zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu kwa mfumo wa BVR, linaendelea vizuri na kusema kuwa muda wa siku saba uliwekwa katika kujiandikisha katika daftari hilo unatosha kutokana na uzoefu uliopatika katika uandikishaji wa majaribio.

Pia waziri mkuu ameiagiza tume ya uchaguzi NEC, kutoa ratiba ya kanda saba zilizogawiwa kwa ajili ya kuwafanya wananchi wasisafiri wakati zoezi hilo litakapofika katika kanda zao.

Aidha Waziri Pinda amevitaka vyama vya siasa na wadau mbalimbali washiriki kwa pamoja katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Katika hatua nyingine Mh. Pinda amezungumzia ukuaji wa uchumi nchini Tanzania na kusema tafiti mbalimbali Afrika na duniani zinaonesha Tanzania ni moja kati ya nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi.

Waziri Pinda ameongeza kuwa serikali kwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imejitahidi kudhibiti mfumuko wa bei ambao kwa kiasi kikubwa ndio chanzo kikubwa cha kuporoka kwa shilingi na kushuka kwa uchumi.

Bunge limeidhinisha bajeti ya ofisi ya waziri mkuu ambayo ni ya jumla ya Shilingi Trilioni Tano, Bilioni Mia Saba Sitini na Tatu, Milioni Mia Saba Themanini na Nne, na Sabini Elfu (5,763,784,070,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Saba, Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu na Tisa Elfu (177,337,309,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.