Jumanne , 30th Jun , 2015

Zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, BVR, bado limeendelea kusuasua katika manispaa ya Morogoro, kutokana na ubovu wa vifaa sambamba na wingi wa watu huku muda wa zoezi hilo ukiwa umekaribia kumalizika.

Mkazi wa Morogoro akiandikishwa katika moja ya vituo

Zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, BVR, bado limeendelea kusuasua katika manispaa ya Morogoro, kutokana na ubovu wa vifaa sambamba na wingi wa watu huku muda wa zoezi hilo ukiwa umekaribia kumalizika.

Eatv imetembelea maeneo mbalimbali na kubaini uchache wa mashine hizo, huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamejitokeza kujiandikisha bila mafanikio, ambapo wananchi wameiomba serikali kuongeza muda wa zoezi hilo, ili kutoa nafasi kwa wengi kushiriki na kupata haki yao ya msingi, na wengine kuwalalamikia waendeshaji wa zoezi hilo kushindwa kufanya kazi zao kwa weledi.

Waendeshaji wa zoezi hilo wamekataa kutoa Ushirikiano kwa waandishi wa habari kutokana na masharti waliyodai kupewa na viongozi wao wa juu, lakini watendaji wa kata na mstahiki Meya wa manispaa ya Morogoro Amiri Nondo wamekiri changamoto ya uchache wa mashine hizo.

Meya Nondo ameahidi kuwa tatizo hilo linashughulikiwa ingawa amekemea na kuonya tabia ya baadhi ya wanasiasa kusababisha vurugu katika vituo vya kujiandikisha na wananchi wanaokwenda kujiandikisha katika mitaa ambayo hawaishi.