Jumanne , 17th Mei , 2016

Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu, Chiku Galawa, ameuhakikishia umma kuwa tatizo la uhaba wa dawati kwenye halmashauri zilizopo mkoani kwake litamalizika ifikapo Juni 30.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa.

Galawa amebainisha hayo alipozungumza na wanahabari na kubainisha kuwa ameridhishwa na mikakati mbalimbali ya kukamilisha utengenezaji madawati kwenye halmashauri zote.

Amesema kwa mkoa mzima wa Songwe mahitaji ya madawati ni 63,537 ambapo yaliyopo ni 49,692 hivyo pungufu ni madawati 11,804.

Ameitaja halmashauri ya wilaya ya Momba yenye jumla ya shule 75 za msingi kuwa yenye upungufu mkubwa wa madawati 4,600 ambapo mahitaji halisi ni madawati 10,111 na yaliyopo ni 5,511 na mkakati uliopo ni kukamilisha ifikapo Mei 30 mwaka huu.

Amesema halmashauri ya wilaya ya Mbozi yenye shule 160 inafuatia kwa kuwa na pungufu ya madawati 3,618,mahitaji halisi ni 30,738 na yaliyopo ni 27,120 na michango na maombi kwa wadau yatakamilika ifikapo Juni 30.

Halmashauri ya wilaya ya Ileje yenye shule za msingi 83 ina upungufu wa madawaati 2,224 ambapo mahitaji halisi ni 13,078,yaliyopo ni 10,854 na tayari yanatengenezwa 1,380 na hadi kufikia Juni 30 yote yatakamilika.

Halmashauri ya mji wa Tunduma iliyo na shule za msingi 25 ina pungufu ya dawati 1,362,mahitaji halisi ni 9,610 na yaliyopo ni 6207 ambapo madawati 455 yanaendelea kutengenezwa.

Hata hivyo Mchanganuo huo wa mahitaji ya madawati mkoani Songwe haujumuishi takwimu za wilaya mpya ya Songwe iliyoanzishwa hivi karibuni.