Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo.
Prof. Muhongo amesema hayo wakati ya ziara ya Ukaguzi wa njia hiyo Mpya inayosafirisha umeme kutoka Mkoani Iringa hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa na baadae kuelekezwa hadi mipakani.
Waziri huyo wa Nishati amesema kuwa Taifa lolote linalotegemea kukua kiuchumi kupitia Viwanda, na Kilimo halina budi kuwa na umeme wa uhakika ikiwa ni pamoja na kuuza umeme au kununua umeme kutoka nchi jirani.
Mhe. Muhongo ameongeza kuwa lengo la kutengeneza njia hiyo ni pamoja na kujiandaa kuwa nchi ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa Umeme Afrika Mashariki ambao unaweza kuwa chanzo kikuu cha kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake mratibu wa Mradi huo James Khalid, amesema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 23 zimetumika kulipa fidia kwa watu wote walioathirika na mradi huo ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.