Ijumaa , 20th Dec , 2019

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa, amesema kuwa Jeshi hilo linamshikilia Afisa wa Elimu kwa Umma wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti kwa sababu za kiupelelezi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Disemba 20, 2019, majira ya saa 11:00 Jioni, Kamanda Mambosasa amesema kuwa wanamshikilia kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili, ambazo hazitasemwa hadharani.

"Ni kweli tunamshikilia kwa sababu za kiupelelezi kuna tuhuma mbalimbali ambazo zinawahusu, hazitasemwa hadharani tunaendelea na upelelezi, tunamshikilia yeye pamoja na wenzake watatu" amesema Kamanda Mambosasa.

Tito Magoti amekamatwa leo majira ya saa 10:00 asubuhi, maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa mashuhuda wameeleza kuwa, watu waliomchukua walikuwa katika gari aina ya Harrier yenye rangi ya maziwa na baada ya hapo walielekea njia ya Posta.