Jumatano , 7th Feb , 2018

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Katibu wake mkuu Dkt. Vicent Mashinji kimelaani vikali kitendo cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa mgombea wao wa Udiwani Muleba Nelson Makoti na kudai wanakosa imani na Polisi juu ya hilo

Dkt. Mashinji amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam baada ya kupita siku kadhaa tokea alipopatikana mgombea huyo akiwa katika hali mbaya jambo ambalo liliwashtua CHADEMA kwa maana mtu huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mwishowe kupatikana lakini akiwa mwenye majeraha mengi mwili mwake.

"Sisi kama chama tunaalani kitendo cha mgombea wetu Mhe. Makoti kutekwa, kuteswa, kunyanyaswa, kuonewa, kulazimishwa ajitoe katika kugombea, wakati ni haki yake kidemokrasia katika Taifa hili. Hili tunalilaani pia tunalaani kitendo cha polisi waliyokuwepo katika eneo husika na kutochukulia suala hili kwa umakini unaohitajika, hiki ni kitendo kisichokubarika", amesema Dkt. Mashinji.

Pamoja na hayo, Dkt. Mashinji ameendelea kwa kusema "nina imani hata huku kuumizwa alipokuwa napo kwa sasa huenda walingeliwahi huyu mgombea wetu asingeumia kwa kiasi hichi alichokuwa nacho sasa hivi. Tunalitaka Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa haraka katika hicho kitendo na itoe taarifa mapema ili tuweze kujua ni nani amehusika na aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria".

Kwa upande mwingine, Dkt. Mashinji amedai wamepewa taarifa kutoka katika hospitali anayotibiwa diwani huyo kwamba anatarajiwa kupewa rufaa ili aweze kuenda katika hospitali nyingine kupewa matibabu zaidi.