Jumanne , 19th Sep , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wakazi wa Kilwa Masoko kuchangamkia fursa zinazotokana na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa ili waweze kupata ajira sambamba na kukuza kipato.

Akizungumza katika uwekaji Jiwe la Msingi la ujenzi wa Bandari hiyo, Rais Dkt. Samia amesema zaidi ya shilingi bilioni 266 ambazo zimetokana na mapato ya ndani zimetumika kwaajili na ujenzi wa bandari hiyo hivyo wakazi wa Kilwa Masoko wanapaswa kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuweza kukamilisha mradi huo kwa ufanisi zaidi.

"Bandari hii inaweza kuzalisha ajira zaidi ya elfu ishirini, hivyo ni wito wangu hususani kwa Wanakilwa kutumia fursa zitakazojitokeza na miradi hii, mzitumie ili tuweze kupata ajira lakini pia kukuza kipato" 

Aidha Rais Dkt. Samia amesema mradi huo unatarajia kuchukua miezi 24 ya ujenzi na mwaka mmoja wa uangalizi na hivyo kufanya jumla ya miezi 36 hadi kukamilika kwake jambo ambalo linahitaji uvumilivu na subra ili mradi uanze kufanya kazi.

"Muda huu kwa watu wanaosubiri wenye hamu ya kuona bandari inakamilika inatumika ni muda mrefu sana, lakini kwenye shughuli za ujenzi na ujenzi makini huu ni muda mfupi sana kwahiyo ndugu zangu tunachoomba kwenu ni ushirikiano kwa serikali mradi huu ujengwe kama ulivyokusudiwa ili uje kuleta manufaa" alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Katika hatua nyingine Rais Dkt. Samia amewataka watumishi wa halmashauri ya Kilwa wakiwemo madiwani na wenyeviti wa halmashauri kutumia vizuri fedha za maendeleo zinazopelekwa katika halamashauri hiyo na kuacha kuzitumia kwaajili ya manufaa yao binafsi.

"Ndogo ndogo ninazozipata zinazotokana na utendaji wa madiwani na wenyeviti wa halmashauri na wenzao katika utekelezaji wa miradi niwaambie tu kwamba hizi fedha zinaletwa kwaajili ya kuondosha dhiki na changamoto za wananchi, hizi fedha haziletwi viongozi mjinufaishe bali zikatutue changamoto na adha kwa wananchi na ndiyo maana nasema mtiririko huu wa fedha Kilwa isipobadilika viongozi kaeni mjitazame kuna nini ndani yenu." alisisitiza Rais Dkt. Samia

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema ujenzi wa bandari hiyo unakwenda kuinua uchumi wa taifa kupitia sekta ya uvuvi ambayo imedhamiria kukuza sekta hiyo kutoka asilimia 1.8 hadi kufikia asilimia 10 kufikia mwaka 2036.

"Tumeadhimia uchumi wa taifa hili uinuliwe kutoka asilimia 1.8 sekta ya uvuvu ufike mpka asilimia 10 katika miaka hii ya kutoka hapa tulipo mpaka 2036, Mhe. Rais hiyo itapatikana kwa kuwavuta wawekezaji wenye meli kubwa duniani waweze kuja kufunga gati katika bandari ya Kilwa Masoko na kuinua uchumi wa Kilwa pamoja na kanda yote ya Pwani ya Kusini.