Jumatatu , 19th Aug , 2019

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson, amesema anampango wa kugombea Ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2020, lakini hajabainisha atagombea jimbo gani, kwa kile alichodai chama chake cha CCM, kinamzuia kutaja jimbo atakalogombea.

Naibu Spika Tulia Ackson, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa BreakFast cha East Africa Radio, wakati akijibu swali la juu ya kuonekana kuonesha nia ya kugombea Ubunge, kwenye jimbo la Mbeya Mjini.

"Mwenyezi Mungu akitupa Uhai 2020 nitagombea, ila nitagombea wapi? naomba watulie kwa sababu chama chetu kina utaratibu wake ila nashukuru ninavyoonekana nina uwezo wa kugombea maeneo mengi." amesema Tulia Ackson.

"Pale Mbeya Mjini kuna ofisi ya Tulia Trust, kwa hiyo wananchi wakisikia umefanya maeneo mengine, pale Mbeya maombi yanakuwa ni mengi, lakini kuhusu watu kufikiri mimi nataka Jimbo, siwezi kusema chochote." amesema Naibu Spika Tulia.

Naibu Spika Tulia Ackson ni miongoni mwa wadau wakubwa ambao wamejitokeza kuunga mkono, Kampeni ya Namthamini inayoendeshwa na East Africa Television na East Africa Radio, yenye lengo la kumsaidia binti aliyepo shuleni kupata taulo za kike, na tayari kwa miaka miatatu ya mwanzo imeshawafikia wanafunzi zaidi ya 5000.