Jumatatu , 8th Apr , 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote, Bara na Visiwani kuendelea kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

“Kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wao makini ambao umekuwa chachu ya kudumisha muungano wetu.”

Ameyasema hayo leo (Aprili 8, 2024) wakati akizindua nembo na kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. “Muungano huu ni tunu adimu na adhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Hivyo basi kila mmoja awe mlinzi.“

Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano yamebeba kaulimbiu isemayo, “Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’ Tumeshikamana na Tumeimarika, kwa Maendeleo ya Taifa Letu’’. 

Amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao kutimiza miaka 60. “Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla.“

Waziri Mkuu amesema kilele cha sherehe za muungano kitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia maadhimisho hayo.

“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.“

Aidha, Waziri Mkuu amesema nchi itaendesha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, hivyo ametoa rai kwa wapigakura wote wahakikishe wanajiridhisha na kushiriki taratibu za kuwafanya kuwa na sifa za kushiriki kuchagua viongozi wenye uwezo na wenye nia njema na Muungano.