Jumatatu , 7th Nov , 2016

Mgombea wa urais kupitia chama cha Republican Donald Trump ameishambulia jamii ya Wasomali wanaoishi katika jimbo la Minnesota nchini Marekani akiwalaumu kwa kueneza maoni yenye itikadi kali nchini humo.

Donald Trump

Bw. Trump ametumia mfano wa kisa cha shambulio la kisu lililotekelezwa na muhamiaji raia wa Somalia mnamo mwezi Septemba katika mji wa Saint Cloud akisema wakaazi wa Minnesota wameteseka vya kutosha.

Bwana Trump ambaye alikuwa katika ziara ya kampeni kabla ya uchaguzi wa Jumanne amesema, kuwa iwapo atakuwa Rais atahakikisha kuwa wakazi wa maeneo hayo wanashauriwa kabla ya wakimbizi kupelekwa ili kuishi.

Hii si mara ya kwanza kwa mgombea huyo kuwashambulia wahamiaji nchini humo ambapo amewahi kukaririwa akisema atawatimua wahamiaji wote wasiokuwa na vibali vya kuishi nchini Marekani na pia atajenga ukuta kuwazuia wahamiaji kutoka Mexico.

Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika kesho Jumanne Novemba, 8 .