Utawala wa Trump umesema Saudi Arabia itaongeza mipango yao ya uwekezaji kutoka dola bilioni 600 hadi takriban dola trilioni 1. Riyadh imekubali pia kununua ndege za kivita na vifaru karibu 300 vya Marekani.
Akihojiwa na waandishi wa habari, Trump alimtetea Bin Salman na kusema Mwanamfalme huyo hakuwa na taarifa zozote kuhusu mauaji ya mwaka 2018 ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliyeuawa ndani ya Ubalozi wa Saudia mjini Istanbul.
Maoni ya Trump yalionekana kupingana na tathmini ya kijasusi ya Marekani mwaka 2021 ambayo ilisema kwamba mwanamfalme huyo alikuwa ameidhinisha operesheni iliyosababisha kifo cha Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul mwaka 2018.
Mwanamfalme huyo, ambaye amekana shutuma dhidi yake, alisema katika Ikulu ya White House kwamba Saudi Arabia ilifanya mambo yote sahihi kuchunguza kifo cha Khashoggi, ambacho alikiita kibaya.
Hii ni ziara yake ya kwanza ya Marekani tangu mauaji hayo, ambayo yalisababisha mshtuko katika uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia.
