Ijumaa , 28th Mar , 2014

Mtu mmoja amekufa papo hapo na wengine watano kujeruhiwa baada ya treni ya mizigo iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kwenda Kigoma kusombwa na maji katika eneo la Gode Gode Mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dk. Shaaban Mwinjaka ameiambia East Africa Radio kwa njia ya simu kwamba ajali hiyo imesababishwa na maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha yaliopelekea treni kuacha njia kutokana na kusomba eneo la reli na hatimae kupinduka.

Wakati huohuo, hali ya miundo mbinu katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania sio ya kuridhisha kutokana na barabara nyingi za Jiji kujaa maji na kushindwa kupitika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mwandishi wa East Africa Radio ameshuhudia barabara kadhaa zikiwemo za Kawawa na Mwai Kibaki zikiwa zimejaa maji kati kati ya barabara huku magari yakionekana kushindwa kupita na kuzimika kutokana na kuwepo kwa madimbwi makubwa ya maji yaliyosababishwa na kuziba kwa mifereji ya kupitisha maji hayo.

Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamesema serikali imekuwa na viongozi ambao ni wasemaji tu lakini si watendaji kutokana na kutoa ahadi zisizotekelezeka na ndio sababu ya kuendelea kuharibika kwa barabara hizo kila mvua zinaponyesha.