Ijumaa , 22nd Jan , 2016

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora alifanya ziara ya kutembelea Shirika la Posta Tanzania ili kufahamu utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu ya Shirika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora

Katika ziara hiyo Prof. Kamuzora aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Maria Sasabo na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Shirika hilo.

Katika ziara hiyo Prof. Kamuzora alimuagiza Kaimu Posta Masta Kuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndugu Fortunatus Kapinga kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato yote ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) nchi nzima yanafanyika kwa kutumia njia ya elektroniki ambapo alisema kuwa, “Shirika liboreshe mifumo yake ya kielektroniki ili kupunguza mianya ya wizi na upotevu wa fedha za Shirika na kufanikisha ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Serikali”.

Prof. Kamuzora aliongeza kuwa Shirika la Posta Tanzania liendane na mabadiliko ili liende kuwahudumia wananchi wa sasa na wa vizazi vijavyo. Shirika ni la kipekee na lina nafasi nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo Shirika kama hili linafanya kazi nzuri kwenye nchi ya China na Brazil.

Aidha, Prof. Kamuzora aliwaagiza Viongozi wa wasimamizi wa Shirika la Posta Tanzania kutumia Sheria, Kanuni na taratibu za kuwasimamia wafanyakazi na kuwachukulia hatua kali na za kinidhamu watumishi wazembe; wasiotimiza majukumu yao; wasio waaminifu na wabadhirifu.

Aliongeza kuwa watendaji wafanye kazi na kusimamia Shirika kwa kuwekeana malengo kama inavyojulikana kisheria kwa kutumia Mfumo wa wa Wazi wa Upimaji Utendaji Kazi (OPRAS). Alisisitiza kuwa, “Sheria zilizopo zinatosha kumsimamisha mtumishi kazi kwa makosa na hatimaye kumfukuza kazi kwa kuwa watumishi wazembe na wasio waadilifu wanawafanya wananchi wawe na mtazamo hasi na Serikali yao”.