Jumatatu , 12th Sep , 2016

Tetemeko dogo la ardhi limetokea tena jana majira ya saa nne usiku katika mkoa wa Kagera na kuzusha hofu kwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba ambao iliwalazimu wengine kulala nje kuhofia uhai wao.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole baadhi ya majeruhi wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera wakati alipotembelea hospitali ya mkoa wa Kagera.

Habari kutoka mkoani Kagera zinasema kuwa tetemeko hilo halikuwa kubwa kama lililotokea siku ya Jumamosi ambalo lilisababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa.

Tetemeko hilo la awali pia lilisababisha kubomoka kwa nyumba 840 huku nyingine 1264 zikiachwa na nyufa na mabweni ya shule ya sekondari Nyakato yakiharibika kabisa kulikopelekea wanafunzi kukosa mahali pa kulala.

Awali akiongea mara baada ya kutembelea waathirika wa tetemeko hilo Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wakazi ambao nyumba zao zimeharibiwa kutorejea kwenye nyumba hizo kwa kuwa bado haijajulikana kama tetemeko hilo litajirudia au la.