Alhamisi , 29th Sep , 2022

Tanzania inatekeleza mfumo wa Taifa wa uchumi wa kidijitali, ambao utahakikisha sekta zote za uchumi zinatumia TEHAMA huku ikiwezesha mabadiliko ya kidijitali yanayojenga jamii jumuishi ya kidijitali kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (Mbunge)

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (Mbunge), wakati akiwasilisha tamko la kisera la Tanzania katika mkutano wa kimataifa wa mawasiliano Duniani (ITU PP 2022) unaofanyika hapa Bucharest, Romania.

Waziri Nape amesema Tanzania ina Sera ya Taifa ya TEHAMA, ambayo imesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali za uchumi.

Tanzania pia imewezesha ujumuishaji wa kifedha ambao umehusisha idadi ya watu wa Tanzania ambao hawakuwa wanapata huduma za kibenki hasa jamii ya vijijini. Alihusisha mafanikio hayo na ushiriki wa Sekta Binafsi.

Aidha Waziri Nnauye amesema kuwa mipango ya uunganishaji wa Mkongo wa Mawasiliano kwa nchi jirani na zisizo na bandari ni ahadi ambazo Tanzania imekuwa ikizipa kipaumbele sana ambapo  Mkongo wa Taifa unaunganisha nchi zisizo na Bahari kupitia maeneo ya mpakani ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi ukiwa na urefu wa KM 18,000.