Jumatano , 29th Mei , 2024

Tanzania imeshinda tuzo ya Jumuiya ya Habari Duniani ya Mwaka 2024 (WSIS 2024) nchini Uswisi, iliyokabidhiwa kwa Rais wa Internet Society Tanzania, Bw. Nazar Nicholas na Katibu Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Dunia (ITU) Doreen Bogdan-Martin huku ikishuhudiwa na Waziri wa Habari Nape Nnauye

Bw. Nazar Nicholas (katikati) akikabiziwa tuzo ya WSIS 2024

Tuzo hiyo imekabidhiwa usiku wa leo Mei 29,2024 wakati wa Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya Habari (WSIS) kwa mwaka 2024 ambapo ujumbe wa Tanzania umeshiriki Mkutano huo wakiongozwa na Mhe. Nnauye.

Ushindi huo umepatikana kupitia mradi wa Tanzania Digital Inclusion Project uliopo ndani ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) ulioshindanishwa na miradi mingine 90 kutoka nchi mbalimbali inayogusa eneo la upatikanaji wa habari na ujuzi.

Mradi wa Tanzania Digital Inclusion Project una miaka mitatu katika utekelezaji wake na unasimamiwa na Society Tanzania na unajihusisha na kuunganisha watumiaji wa intaneti ya kasi inayotumia mfumo wa “ushirikabando” ambapo mpaka sasa Shule (10), ofisi ya Serikali ya mtaa (1), Ofisi ya Serikali ya Kata (1), kituo cha polisi (1), Community Center (1) na  vikundi 6 vya Wajasiriamali vimeunganishwa. 

Kupitia mradi Tanzania Digital Inclusion Project mafunzo ya kidijitali yametolewa kwa wananchi 1200 wake kwa waume, waalimu 197 wamepatiwa mafunzo ya mafunzo mtandao (e-learning) wasichana 2000 wameongeza ujuzi na maarifa kwa kuunganisha maeneo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayobadilisha mfumo wa kujifunza.

Rais wa Internet Society Tanzania, Bw. Nazar Nicholas ameishukuru Wizara kwa sera madhubuti ya miundombinu na hasa usambazaji mtandao wa Mkongo wa Mawasiliano kwa zaidi ya kilomita 10,000, na pia  Mradi wa Tanzania ya Kidijitali na mpango wa III wa Maendeleo.