Jumatatu , 1st Aug , 2016

Tanzania inatarajia kuingiza kiasi kikubwa cha pesa za kigeni kufuatia kukamilika na kuanza kazi kwa kiwanda cha LABIOFAM kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani, kinachozalisha dawa za kibaiolojia zinazotumika kupambana na ugonjwa wa malaria.

Baadhi ya mitambo katika kiwanda cha dawa ya kuuwa viluwiluwi vinavyosababisha ugonjwa wa malaria cha LABIOFAM kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani.

Kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano baina ya Shirika la Taifa la Maendeleo NDC na kampuni LABIOFAM SA ya nchini Cuba ambacho kinatengeneza dawa rafiki kwa mazingira, ambazo zinatumika kwa kumwaga maeneo ambayo ni mazalia ya mbu na kuua viluwiluwi ambao wanapokomaa hugeuka mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria.

Kwa mujibu wa Afisa Mauzo wa Kampuni ya Tanzania Biotech Products Ltd inayoendesha kiwanda hicho kupitia ubia wa serikali za Tanzaniua na Cuba Bw. Frank Mzindakaya; hatua hiyo inatokana na Tanzania kuwa nchi pekee barani Afrika yenye kiwanda cha kutengeneza dawa hizo na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kunufaika na soko kwenye nchi nyingine za Afrika.

"Kiwanda hiki ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi kwani dawa zinazotengenezwa na kiwanda hicho zinahitajika sana katika kukabiliana na mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria," amesema Bw. Mzindakaya.

Amesema ugonjwa wa malaria ni janga linalozikabili nchi nyingi za Afrika na hivyo hiyo niu fursa nzuri ya kiuchumi kwani katika kupambana na ugonjwa huo nchi nyingi za Afrika zitakuja kununua dawa hiyo inayozalishwa hapa nchini.

Mzindakaya amesema kwa sasa Kampuni hiyo ipo kwenye mazungumzo na halmashauri za wilaya na miji nchini pamoja na nchi kadhaa wanachama wa umoja wa kupambana na malaria ujulikanao kama ALMA, ambazo zimeonyesha nia ya kununua dawa hizo kwa ajili ya kukabiliana na malaria katika nchi zao.

"Tayari tupo katika mazungumzo na nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Viongozi walio katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ALMA kwa ajili ya nchi hizo kununua dawa hiyo kutoka Tanzania na hivyo kuongeza wigo wa soko la dawa hiyo," ameongeza Bw. Mzindakaya.

Aidha, mbali ya nchi hizo, kiwanda pia kinaendelea na mazungumzo na halmashauri za miji na wilaya nchini kwa ajili ya kuhakikisha kuwa halmashauri hizo zinaanza kununua dawa hiyo kwa ajili ya kuua viluwiluwi na hivyo kupunguza kasi ya ugonjwa wa malaria katika maeneo yao.

"Kiwanda hiki kinatoa mwelekeo sahihi wa jinsi Tanzania inavyoweza kutekeleza mpango wa kuwa taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025...hii inatokana na ukweli kwamba malaria imekuwa ikipunguza nguvukazi kubwa katika uzalishaji na hivyo kwa kutokomeza malaria, Tanzania inauhakika wa kuwa na watu wenye afya bora inayohitajika katika uzalishaji," amefafanua Bw. Mzindakaya.