Jumatano , 29th Jun , 2016

Rais wa Comoro Azali Assoumani, amesema serikali yake itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Comoro katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na biashara.

Makamu wa Rais Bi. wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,akiwa na Rais wa Comoro Azali Assoumani.

Rais huyo wa Comoro ametoa kauli hiyo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais John Magufuli akiwa kwenye mapumziko mafupi kabla ya kuendelea na safari yake ya Mecca – Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Umrah.

Rais Azali Assoumani pia amepongeza jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano zinazolenga kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za kijamii na kusisitiza kuwa serikali yake itaendelea kujifunza kutoka Tanzania ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Comoro.

Akitoa ujumbe wa Rais Magufuli, Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu amemhakikishia rais huyo kuwa Tanzania itadumisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili hasa kwenye sekta za elimu, afya na biashara kwa ajili ya manufaa ya nchi hizo mbili.

Wakati huo huo Mh. Samia, amekutana na kufanya mazungumzo na balozi wa Japan hapa nchini Masaharu Yoshida, na kumweleza kuwa serikali itaendelea kuweka na kuboresha mazingira bora kwa ajili ya wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo wawekezaji kutoka nchini Japan.