Jumatatu , 12th Jan , 2015

Serikali imesema inafanya utaratibu wa kufanya mazungumzo na Serikali ya Kenya ili kuondoa utata unaoigubika sekta ya utalii baada ya kuibuka kwa sakata la magari yaliyobeba wageni kuzuiliwa kuingia katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata.

Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu.

Kusudi la Serikali ya Tanzania kufanya mazungumzo na Kenya linafuatia malalamiko ya tokea Desemba 22 mwaka uliopita kutoka kwa watoaji wa huduma za utalii nchini kuhusu kuzuiliwa kwao kuingiza wageni katika uwanja wa Jomo Kenyata huku sababu za kuzuiliwa kwao zikiwa bado ni kitendawili.

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu akizungumza Jijini Arusha na wafanyabiashara wa utalii ambao wamekutana na kadhia hiyo amesema suala la kuzuiliwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuingiza magari ya wageni katika uwanja wa Jomo Kenyata ni suala ambalo halina maslahi kwa mpande zote.

Nyalandu amesema mahusiano ya biashara ya watalii baina ya nchi hizi mbili ni ya muda mrefu ambapo takwimu zinazoishia kipindi cha mwaka 2014 zinaonesha wageni walioingia nchini kupitia kiwanja cha Ndege cha Jomo Kenyata ni takribani laki mbili na hatua ya kuwekwa kwa vizuizi hivyo kumeifanya Wizara yake kuchukua hatua za haraka za kidipromasia kulitafutia ufumbuzi sakata hilo..

Wakati sakata hili likiibuka,Nchi ya Kenya inatajwa kuwa katika kampeni za kuishawishi Tanzania kuondoa vizuizi katika mpaka wa Borogonja uliopo katika hifadhi za Maasai Mara na Serengeti ambao ulifungwa wakati wa utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiusalama.