Jumatano , 1st Oct , 2014

Tanzania imetajwa kushika nafasi ya 92 katika orodha ya nchi zenye idadi kubwa ya wazee kati ya nchi 96 duniani huku takwimu za taasisi ya Helpage International zikionyesha kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee itakuwa sawa na ya watoto.

Akiongea jijini Dar es salaam wakati Tanzania imejumuika na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya wazee Mkurugenzi wa Taasisi ya Helpage Bi. Amleset Tewodros amesema Takwimu zinaonesha kuwa katika nchi 96 duniani idadi ya wazee ambao wanaanzia umri wa miaka 60 imeongezeka hadi kufikia asilimia 91 ya idadi ya watu duniani huku asilimia 4 tu ya wazee wakipata pensheni ya uzeeni na asilimia 73 wakiachwa huku wengi wao wakitegemea kilimo kama nyenzo ya uchumi wao.

Hata hivyo, Tewodros amesema ukuaji wa uchumi pekee hauwezi kuboresha ustawi wa wazee na kuitaka serikali ya Tanzania kuweka sera zenye kusimamia maslahi na yenye kutoa huduma kwa wazee na kushughulikia matokeo ya uzeeni.

Kwa upande wao wazee Juma Mwita na Amani Mbirikira wamesema serikali haijaonesha jitihada kubwa katika kuwasaidia wazee hasa waliopo katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kuwatunza wazee na kueleza ukosefu wa lishe bora unazorotesha afya za wazee nchini.