Jumatano , 7th Feb , 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ili kukabiliana na changamoto za utengenezaji ajira barani Afrika yanahitajika mageuzi na mbinu jumuishi kwa kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wote husika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 7 wa Wadau wa Kijamii wa Afrika katika masuala ya Kazi na Ajira uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 7 wa Wadau wa Kijamii wa Afrika katika masuala ya Kazi na Ajira uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam, tarehe 07 Februari 2024. 

Amesema linahitajika jukwaa la utekelezaji litakalounganisha mashirika ya serikali, washirika wa ndani ya nchi, sekta binafsi pamoja na wadau wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto za utengenezaji wa ajira.

Makamu wa Rais amesema nchi za Afrika zinapaswa kuongeza ujuzi na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija katika uzalishaji badala ya kuona teknolojia ni adui kwa usalama wa ajira. Amesema ujio wa Akili Mnemba (Artificial Intelligence) utaathiri utengenezaji wa ajira kwa kupunguza ajira ndogondogo zilizopo na kutengeneza ajira mpya hususani zinazohitaji ujuzi wa kiufundi.

Makamu wa Rais amesema matumizi ya Akili Mnemba yanazitaka Serikali na sekta binafsi katika bara la Afrika kutoa kipaumbele kwa kuwapa wafanyikazi ujuzi wa juu zaidi wa kiteknolojia ili kuwawezesha kuendana na soko jipya la ajira. 

Ametoa wito kwa Mkutano huo kujadili umuhimu wa mafunzo mapya kwa wafanyakazi, kufanya uchambuzi, kutambua sekta ambazo zina uwezekano wa kupoteza idadi kubwa ya fursa za ajira na sekta ambapo Akili Mnemba itaongeza ajira za ujuzi wa juu. 

Amesema eneo moja mahususi ambalo Akili Mnemba inaweza kusaidia kutengeneza ajira ni utafiti wa kilimo unaolenga kuboresha aina za mbegu zenye mavuno mengi na mbegu zinazostahimili ukame ambazo zitachochea tija kubwa na ajira za baadaye.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa Mkutano huo kujadili hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake ikiwa ni pamoja na mbinu jumuishi zinazolenga kulinda maisha ya jamii na kuimarisha ulinzi wa mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema mabadiliko ya tabianchi kwa upande mwingine yana fursa nyingi katika kutengeneza ajira Barani Afrika ikiwemo katika mchakato wa kupunguza athari, kuna ajira ambazo zinatengenezwa hususani pale wakulima wanapotumia kilimo hai na utafutaji na ukuzaji wa mbegu na malisho kwa jamii za wafugaji. 

Vile vile, amesema katika mapinduzi ya kijani kuna fursa za ajira zilizoundwa kwa kuweka kipaumbele kwa nishati safi hususani nishati jua, jotoardhi, upepo na maji.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imedhamiria kutengeneza ajira milioni 7 kati ya mwaka 2020-2025 ambapo mikakati ya utekelezaji wa lengo hilo ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara, uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi katika halmashauri zote za wilaya nchini zenye miundombinu inayohitajika kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili kufanya shughuli za uzalishaji mali. 

Amesema mikakati mingine ni pamoja na kutoa mafunzo na kuwaunganisha vijana na taasisi zinazotoa mikopo nafuu ikiwemo kuanzisha programu ya Jenga Kesho Bora: Mpango wa Vijana kwa Biashara ya Kilimo (BBT-YIA) na ile ya Sekta ya Mifugo (BBT-Live) kwa ajili ya uzalishaji wa nyama ya ng' ombe na ufugaji wa Samaki. 

Pia uanzisha vituo vilivyotengwa ambapo vijana wataweza kujifunza na kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujihusisha na uzalishaji pamoja na kutenga asilimia 10 ya mapato ya kila halmashauri ya wilaya kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum.

Mkutano huo unafanyika tarehe 7-8 Februari 2024 umeandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa Kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Waajiri (IOE).