Jumanne , 7th Jul , 2015

Tanzania ipo nyuma katika utumiaji wa mbegu bora za watafiti wa mazao ya kilimo, ambapo asilimia 25 tu ya mbegu hizo, hutumiwa na wakulima na kusababisha upatikanaji hafifu wa mazao, ukilinganisha na nchi zingine za Afrika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal.

Akizungumza jijini Arusha, Makamu wa Rais Dkt. Gharib Bilal wakati akifungua mkutano wa kidiplomasia kwa ajili ya kufikia itifaki ya ulinzi wa watafiti wa mimea tofa nchi za Afrika, ili wapate haki stahili, amesema utumiaji wa mbegu bora unaleta tija kwa wakulima endapo utazingatiwa.

Amesema watafiti wamekutana Arusha ili kufikia itifaki, itakayohamasisha watu kufanya utafiti zaidi, kwa ajili ya kutafuta mbegu bora zitakazostahimili katika nchi za Afrika.

Dk. Bilal amesema wakulima wengi Tanzania wanatumia mbegu za mazao waliyolima, badala ya kutumia za watafiti na matokeo yake hupata mazao hafifu.

Amesema katika mkutano huo wanatarajia kuweka itifaki itakayolinda watafiti wa mbegu kuwa na hati miliki ya ugunduzi wao wa mbegu bora, tofauti na ilivyo sasa.

Naye Waziri wa Kilimo,Chakula na ushirika, Stephen Wasira, amesema utafiti wa kilimo lazima ufanywe na nchi zote kwa kushirikiana na wagunduzi, ili waweze kupata mbegu bora.

Akitolea mfano amesema Tanzania inawatafiti wazuri wa Kahawa kutoka TACRI, ambao wamegundua mbegu inayostahimili magonjwa, tofauti na kahawa za zamani mkulima alijikuta akitumia gharama kubwa kununua dawa za kupambana na magonjwa.

Amesema hivyo endapo utapatikana ulinzi wa wagunduzi wa mbegu, ukipatikana utaimarisha zaidi umoja wa watafiti hao.