Ijumaa , 8th Jul , 2016

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade imetakiwa kuandaa maonyesho ya biashara katika kila mkoa nchini ili kutoa fursa kwa wabunifu na wajasiriamali wa maeneo hayo kuonyesha kazi zao.

Akiongea na East Africa Radio jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la Viwanda Vidogo nchini SIDO Mhandisi Omary Bakari amesema ili kuwepo na mapinduzi ya kweli ya viwanda ni vyema wavumbuzi na wajasiriamali wakapewa nafasi ya mara kwa mara kuonyesha kazi zao.

Mhandisi Bakari amesema, maonyesho yanatoa fursa kwa wabunifu kutambua mahitaji ya watanzania pamoja na kutambulisha bidhaa mpya kwa wateja sambamba na kupanua wigo wa masoko kwa wajasiriamali.

Aidha, Mhandisi Bakari amewataka wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali walio pata fursa ya kushiriki maonyesho hayo, watumie nafasi hiyo kujifunza jinsi ya kuboresha, kuhifadhi bidhaa zao na kutafuta masoko.