Jumamosi , 25th Jul , 2015

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Iringa imewatahadharisha wagombea wa vyama vya siasa katika ngazi ya ubunge na udiwani kutotumia rushwa katika kampeni zao.

Mkuu wa Takukuru Iringa Bi Eunice Mmari akiongozi mkutano huu uliowakutanisha wagombea ubunge na Udiwani.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Iringa Bibi. Eunice Mmari amesema wagombea watakaobainika kutoa au kufanya vitendo vinavyoashiria rushwa kuwashawishi wananchi wawachague watachukuliwa hatua za kisheria.

Bibi Mmari amesema taasisi hiyo itakusanya taarifa za kila mgombea kwa vyama vyote vya siasa ili kubaini wanaotumia rushwa kwa ajili ya kupata kura kwa wananchi wao.

Amewashauri wananchi kutoa taarifa kwa taasisi hiyo pindi wanapoona mgombea anatoa rushwa kwa ajili ya kuwashawishi wananchi kuwachagua.

Baadhi ya wagombea wa ubunge jimbo la Iringa Mjini kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Agustino Mahiga na Bw. Frank Kibiki wameshukuru TAKUKURU kwa kuwakumbusha maadili ya uchaguzi.

Hata hivyo, Bibi Mmari amewakumbusha wananchi kutochagua viongozi wanaotumia rushwa kwani hawatawaletea maendeleo ya kweli.

Wagombea wa ubunge na udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Iringa Mjini wameendelea kufanya kampeni kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Baadhi ya wagombea hao wameahidi kutatua kero mbalimbali za wananchi ikiwa watapitishwa na chama chao.

Wagombea 13 wa Chamba Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Iringa Mjini ambao ni Mahamudu Madenge, Nuru Hepautwa, Fales Kibasa, na Peter Mwanilwa.

Wengine ni Bw. Mwilinge, Balozi Agustino Mahiga, Bibi Jesca Msambatavangu, Bw. Fredrick Mwakalebela, Bw. Aidan Kiponda, Bw. Michael Mlowe, Dkt. Yahaya Msigwa na Addo Mwasongwe.

Hata hivyo, zoezi la kufanya kampeni kwa wagombea wa ubunge limeanza katika kata za nduli, Kihesa, Mkwawa na litahitimishwa Julai 31, katika kata ya Gangilonga.