Jumatano , 26th Nov , 2014

Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya juu nchini (TAHLISO) imetangaza maandamano makubwa yasiyo kuwa na kikomo kuelekea Bungeni kwa ajili ya kuishinikiza serikali iwapatie mkopo wanafunzi ambao walidahiliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini.

Mwenyekiti wa Tahliso Taifa, Musa Mdede

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Tahliso Taifa, Musa Mdede amesema maandamano hayo yatakuwa na lengo moja tu la kuishinikiza serikali kuwapatia mkopo vijana elfu 28 ambao wameshindwa kujiunga na vyuo kwa ajili ya kukosa mkopo.

Amesema kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya mikopo nchini vijana waliodahiliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini ni 58,037 ambapo waliotakiwa kupata mkopo ni 30,000 ambao ni sawa na asilimia 51 huku ambao wangekosa mkopo huo ni vijana 28,037 ambao ni sawa na asilimi 49 lakini  waliokosa mkopo ni nusu ya wanafunzi wote waliodahiliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Kwa upande wake Rais wa chuo kikuu cha St. John’s cha mjini Dodoma, Daniel Damian amesema kuwa serikali ina wajibu wa kuwapatia mkopo wanafunzi wote wanaotakiwa kujiunga na vyuo na kwamba maandamano hayo yana lengo ya kuishinikiza serikali kumpa mkopo kila mwanafunzi mwenye sifa ya kujiunga na chuo.

Mbali na hilo amezipongeza nchi wahisani waliokatisha misaada yao kwa Tanzania kutokana na kashfa hiyo ya Escrow na kusema hiyo iwe fundisho kwa serikali kuwa fedha hizo hazikuwa za mtu binafsi bali ni za umma.