Jumamosi , 16th Aug , 2014

Waziri mkuu wa zamani nchini Tanzania Fredrick Sumaye amependekeza kusitishwa kwa mjadala wa katiba mpya unaoendelea mjini Dodoma kwa kuwa inaonekana dhahiri kuwa si muda muafaka wa kupata katiba mpya kwa sasa.

Waziri Mkuu wa zamani Fredrick Sumaye.

Amesema kusitishwa kwa mjadala huo kutatoa fursa kwa watanzania kujipa muda zaidi wa kutafakari ili kufanikisha upatikanaji wa katiba muafaka kwa wakati unaofaa.

Kauli hiyo ya waziri mkuu wa zamani imekuja wakati bunge hilo linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma vinavyohudhuriwa na wajumbe wengi kutoka chama cha Mapinduzi CCM.

Wakati huo huo Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umesema Rais Kikwete ndiye anayeweza kulitolea ufafanuzi suala la kusitisha Bunge Maalum la Katiba na siyo mtu mwingine.

Umoja huo pia umeendelea na msimamo wa kumtaka Rais kuwasiliana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kulisitisha.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa CHADEMA, John Mnyika, ameiambia East Afrika Radio kwa njia ya simu kufuatia kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambaye alisema kwamba hakuna kifungu cha sheria kinachomwezesha Rais kulisitisha Bunge hilo.

Mnyika amesema Rais katika hotuba yake ya Julai mwaka huu alitoa ahadi ya kuingilia kati mazungumzo ya vyama vya siasa nchini endapo yatakwama.