Washirika wa karibu wa Waziri Mkuu nchini Uingereza, Keir Starmer, wamesema, kiongozi huyo anapinga vikali mipango yoyote ya kujaribu kumwondoa madarakani.
Kauli hiyo imekuja, wakati huu kukiwa na hofu kuwa, kazi ya Waziri Mkuu Starmer, ipo hatarini, na hili huenda likashuhudiwa baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya serikali, wiki mbili zijazo.
Ripoti za ndani zinasema, kuwa washrika wa Waziri Mkuu Keir wana mashaka makubwa kuwa, kuna mpango ndani ya chama tawala cha Labour kumwondoa katika nafasi hiyo.
Wanaotajwa kuwa huenda wakachukua nafasi hiyo ya bwana Starmer ni pamoja na Waziri wa afya Wes Streeting na Waziri wa Mambo ya ndani Shabana Mahmood.
Kwa miezi kadhaa sasa, idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala cha Labour, wamekiri kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa serikali kupata mtikisiko mkubwa, baada ya uchaguzi wa majimbo huko Scotland na Wales, na ule wa serikali za mitaa katika baadhi ya maeneo nchini Uingereza mwezi Mei.
Kura za maoni zinaonyesha kuwa Keir hapendwi na hana umaarufu mkubwa, pengine kwa siku za hivi karibuni ni waziri mkuu wa Uingereza asiyekubalika kabisa katika historia ya kura za maoni.

