Alhamisi , 1st Jul , 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa yote nchini kuhakikisha siri za serikali hazisambai hovyo kwenye mitandao ya Kijamii kutokana na baadhi ya barua za serikali kukutwa kwenye mitandao ya kijamii.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa

Mhe. Majaliwa amesema hayo Jijini Dodoma mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa na kuwaambia viongozi hao kuwa wanaowajibu wakulinda siri za serikali hivyo kuwataka kusimamia na kudhibiti utunzaji wa siri za serikali katika maeneo wanayofanyia kazi.

Waziri Mkuu amesema kumekuwepo na tabia kwa barua za serikali kuonekana kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, Instagram, twitter jambo hili ni aibu na sio usiri wa nyaraka za serikali, hakikisheni mnalinda na kudhibiti utandawazi uliopo katika suala la utunzaji wa siri za serikali.

Pia Mhe. Majaliwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia watumishi wa umma hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili waweze kutunza siri za ofisi na kuwaelekeza kutumia mfumo unaokubalika katika utoaji wa taarifa na usambazaji wa nyaraka za serikali

Wakati huo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu amesema wataleta mapendekezo ya kuwapima wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wote nchini kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi.