Jumatano , 22nd Mar , 2023

 Imeelezwa kuwa kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi ikiwamo uchimbaji wa madini na uvuvi mkoani Simiyu, umesababisha ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) mkoani humo.

Mratibu wa Kudhibiti ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Simiyu, Emmanuel John, ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Mjini Bariadi.

“TB kwenye Mkoa wa Simiyu inaongezeka (maambukizi) kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi, hususani wachimbaji wadogo wadogo wa madini na kambi za uvuvi kule Busega. Mwaka jana tulikuwa na wagonjwa 3,600 ikilinganishwa na mwaka juzi ambapo tulikuwa na wagonjwa 2,700,” amesema Emmanuel.

Mratibu huyo ameogeza kwamba kwa mujibu ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa mwaka 2021, Tanzania ilikuwa na watu 132,000 walioambukizwa ugonjwa huo, na kwamba mpango wa Taifa ni kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, jamii imeshauriwa kuchukuwa tahadhari kwa kuvaa barakoa kwenye msongamano wa watu, ili kuepusha na hatari ya maambukizo ya ugonjwa huu wa Kifua Kikuu.