Jumamosi , 16th Mei , 2015

Kutokana na machafuko yanayoendelea nchini Burundi hadi kusababisha kufurika kwa waomba hifadhi nchini hususani katika mkoa wa Kigoma, kambi ya nyarugusu iliyopo wilaya ya Kasulu imeamua kufunga shule zilizopo ndani ya kambi hiyo ili kupata nafasi.

Waomba hifadhi toka nchini Burundi wakiwasili kwa boti, Mkoani Kigoma.

Mkuu wa kambi hiyo, Sospeter Boyo, akizungumza na East Africa Radio, amesema uwezo wa kambi hiyo kisheria za kimataifa ni kuhifadhi wakimbizi 50,000 lakini kwa sasa ina wakimbizi 54,706 hao wakiwa ni wa zamani.

Boyo amesema hadi juzi wamepokea wahifadhi wapya 16,808 ambao wameanza kupokelewa baada ya serikali kuagiza hivyo tangu Aprili 29 mwaka huu hivyo kufikisha watu 71,514 na kusababisha kambi kuelemewa.

Hata hivyo amesema licha ya kufunga shule kambini hapo, lakini huduma muhimu zinapatikana zikiwamo za chakula, madawa na malazi huku serikali ya mkoa wa kigoma ikitoa eneo lingine la kujenga kambi ya pili.

Aidha, amesema wamewasiliana na viongozi wa dini wa makanisa na misikiti ndani ya kambi hiyo ili kuweza kusitisha huduma zao kwa muda, kwa lengo la kuwaweka wakimbizi hao kabla wakati utaratibu wa kuwajengea mahema ukiendelea.

Wakimbizi hao wamekuwa wakiwasili katika kambi hiyo kila siku wakitokea kitogoji cha Kagunga wilaya ya Kigoma wanakochukuliwa na meli ya MV Liemba, baada ya kukimbia machafuko nchini mwao yanayotokana na kupinga Rais Pierre Nkurunzinza kuwania awamu ya tatu ya uongozi.

Awali afisa uhamiaji mfawidhi wa Kagunga, Boniface Mayala, amesema baada ya kutangazwa kuangushwa Rais Nkurunzinza na jaribio hilo kukwama, wameingia wakimbizi 108 na kufikisha idadi ya walioingia nchini mpaka sasa kufikia 90,000.