Jumamosi , 12th Oct , 2024

Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameipongeza Shule ya Sekondari Kinyerezi ya jijini Dar es Salaam kwa kuwalea wanafunzi kwa mrengo wa kisasa hali inayopelekea kuibua na  kukuza  vipaji vingi  

Amesema katika dunia ya sasa kwenye sanaa ndiko kuna  uwanja mkubwa wa ajira

Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Oktoba 12, 2024  wakati akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kinyerezi  iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salam 

"Nimefarijika kuona vipaji vya kila aina, nimewaona  wasanii wenye vipaji vikubwa na pia nimeambiwa kuna mwanafunzi kwa sasa yupo Uingereza alichukuliwa tu mara baada ya kuhitimu masomo yake kutokana kipaji kikubwa alichonacho cha kucheza mpira " amesema .Simbachawene 

Amesema makuzi ya mrengo wa kisasa kwa wanafunzi wa  sasa ni jambo lisiloepukika kwa vile wanafunzi walio wengi wanaohitimu masomo yao hawarudi vijijini kulima 

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewataka wahitimu hao wa kidato cha nne  na wanafunzi wanaoendelea na shule licha ya vipaji walivyonavyo wajitahidi kusoma kwa bidii huku akiwasisitiza kujiepusha kuiga tamaduni za kigeni ambazo haziendani na tamaduni zetu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene amempongeza Rais Mhe.Samia Suluhu Hasssan  kwa kukubali kutoa kiasi cha Sh. Bilioni 28 kwa ajili ya  jiji la Dar es Salaam ili ziweze  kutumika  kwenye  ujenzi wa madarasa
Amesema Serikali ya awamu ya tano  imedhamiria kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu kwenye mazingira bora na ya kisasa ili kuhakikisha hakuna mtoto  anayeachwa nyuma katika kutimiza ndoto zake

Awali, Mkuu wa Shule hiyo,  Daniel Mwaka amesema Shule hiyo licha ya kuwa nyumba ya vipaji lukuki lakini kwenye suala la ufaulu wa masomo imekuwa ifanya vizuri mwaka hadi mwaka

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo,  ufaulu wa wanafunzi  umekuwa ni  zaidi ya asilimia 80 na kusisitiza kuwa  ufaulu wa  wahitimu wa mwaka huu ufaulu utapanda zaidi hadi kufikia  asilimia 93 kutokana na jinsi wanafunzi hao  walivyoandaliwa.