Ijumaa , 5th Aug , 2016

Mwanasheria Jebra Kambole amesema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 pamoja na Katiba ya nchi zinaruhusu shughuli za siasa pamoja na maandamano ila kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

Wakili Jebra Kambole akiwa kwenye kipindi cha HOTMIX

Akizungumza katika kipindi cha HOTMIX kinachorushwa na EATV mwanasheria huyo amesema hakuna sheria ambayo inaonesha ukomo wa shughuli za siasa baada ya uchaguzi bali sheria zilizopo zinaelekeza chama cha siasa kinatakiwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria.

"Ibara ya 26 inaonesha kwamba kila mtu ana jukumu la kuheshimu katiba na kufanya kazi na siasa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, na kuna watu ambao shughuli zao ni siasa kutafuta wanachama wapya kuzungumza na wanachama ni haki yao na hakuna mipaka ya eneo la kufanyia siasa ili mradi sheria ifuatwe’’ Amesema Jebra.

"Kuna vyama ambavyo havina wabunge, havina madiwani haviwezi kukaa kimya hadi uchaguzi, katiba yetu inasema kila mtu ana haki ya kufanya kazi na siasa na kazi pia, kuna watu ni wenyeviti wa vyama vya siasa wao hawawezi kukaa kimya , katiba yetu inasema watu wote ni sawa’’ Amesisitiza Jebra

Aidha Mwanasheria huyo amesema kinachotakiwa , ukitaka kufanya mkutano wa siasa unatakiwa kutoa taarifa kwa muda wa saa 48 kabla ya mkutano kufanyika na ambaye amepewa mamlaka ya kuzuia mkutano wa siasa ni mkuu wa polisi katika eneo husika na sababu atazitoa kimaandishi kama chama hicho hakijasajiliwa au sababu za usalama wa nchi.